![]() |
Baada ya mapambano ya siku mbili
na waandamanaji, polisi wameondoka katika medani ya Taksim mjini
Istanbul na maelfu ya waandamanaji wameikalia medani hiyo.
Hapo awali waziri mkuu wa Uturuki, Reccep Tayyip Erdogan, alitoa wito watu waache kuandamana haraka - maandamano makubwa kabisa kwa miaka kadha. Lakini Bwana Erdogan ameahidi kufanya uchunguzi kuhusu tuhuma kwamba polisi walitumia nguvu nyingi. Nchi kadha zimeeleza wasiwasi kuhusu swala hilo. Chanzo cha maandamano ni mpango wa kujenga maduka katika medani ya Taksim - mpango ambao Bwana Erdogan anasema atautekeleza. Waandamanaji vijana piya wanailaumu serikali kwamba imekuwa ya kimabavu na kuifanya nchi kufuata Uislamu. Msemaji wa serikali alikanusha malalamiko hayo alipohojiwa na BBC na alisema tuhuma zenyewe ni za kushangaza. |
Wanabalozi katika Baraza la
Usalama la Umoja wa Mataifa wanasema kuwa Urusi imezinga mswada wa
azimio la kueleza wasiwasi kuhusu hali, hasa ya raia, kwenye mji wa
Syria wa Qusair ambao umezingirwa.
Mashambulio ya serikali dhidi ya mji huo unaodhibitiwa na wapiganaji yameendelea kwa zaidi ya majuma mawili na wakaazi wamenasa bila ya chakula, maji wala madawa.
Lakini wanabalozi wanasema Urusi haitaunga mkono mswada huo wa azimio kwa sababu Umoja wa Mataifa haukushughulika wakati mji huo ulipotekwa na wapiganaji.
Hapo jana Umoja wa Mataifa na Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu, ICRC, yalitoa maombi kuwa wasaidizi waruhusiwe kuingia Qusair.
Msemaji wa ICRC, Dibeh Fakhir, aliiambia BBC taarifa wanazopata kuhusu hali katika mji huo:
" Ripoti tunazopata zinasema kuna upungufu mkubwa wa maji, chakula na madawa.
Piya zinaeleza kuwa mamia ya raia wamejeruhiwa na hawawezi kupata matibabu.
Maelfu tayari wameshakimbia Qusair na maelfu wanasaidiwa na Shirika la Msalaba Mwekundu la Syria, likisaidiwa na ICRC na mashirika mengine.
Hata hivo inaripotiwa maelfu bado wako ndani ya mji - kati yao ni mamia waliojeruhiwa vibaya lakini haiwezekani kuwatibu"
Alisema kuweza kusaidia inavyotakiwa, ICRC inahitaji kuwepo Qusair bila ya kuingiliwa kati na serikali.



































